Kamati Ndogo ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama Taifa, leo Agosti 27, 2024 imetembelea na kukagua kisiwa cha Tembonyama kilichopo kata ya Kirongwe, kijiji cha Banja kwa lengo la kujiridhisha na hali ya usalama kisiwani hapo kabla ya kuingia mikataba na mwekezaji.
Kamati hiyo inayoongozwa na Meja Jenerali Mbaraka Mkeremy ambaye ni Mwenyekiti, imefika baada ya uamuzi wa pamoja wa wanakijiji cha Banja kupitia Mkutano Mkuu wa kijiji hicho kuomba kutafutiwa mwekezaji ili kijiji kiweze kupata mapato.
Akizungumza na wanakijiji, Meja Jenerali Mkeremy amewataka viongozi wa Wilaya, Kijiji pamoja na wananchi kuzingatia hali ya usalama kisiwani hapo na kijiji kwa ujumla kabla na wakati wa kusainisha mkataba na mwekezaji atakayependekezwa pamoja na kujali maslahi ya wananchi.
" Suala la kwanza ni Ulinzi na Usalama, kama hakuna usalama hakuna kitakachoeleweka" alisisitiza. Walioturithisha nchi hii, waliturithisha ikiwa nzuri na salama, hivyo na sisi tuhakikishe tulichorithishwa tunarithisha na wengine" alisema Meja Jenerali Mkeremy.
Akisisitiza suala la usalama wa kisiwa hicho, Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhe. Aziza Mangosongo ameweka mkazo pia ulipaji mzuri wa kodi kwa Halmashauri ili mwekezaji atakayepatikana, aweze kuzingatia makubaliano na vigezo vyote ambavyo vinatakiwa na Wilaya na Taifa kwa ujumla kukwepa upoteaji wa mapato.
Kwa upande wao, wakazi wa Banja wameishukuru Serikali kwa hatua hiyo na kuahidi kutoa ushirikiano ili kuleta maendeleo katika sekta ya utalii wilayani.
" Kwa niaba ya wazee wa kijiji cha Banja, natoa shukrani nyingi kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tumefurahishwa na wageni wetu, hivyo karubuni sana" alisema Mzee Mohammed Uledi.
Kisiwa cha Tembonyama kina ukubwa wa ekari 35 na kinatarajiwa kupata mwekezaji atakayeleta mchango mkubwa katika masuala ya utalii, ikiwa ni mwendelezo wa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukuza utalii nchini huku utunzaji wa mazingira ukipewa kipaumbele.
Shughuli mbalimbali zinazofanyika kisiwani hapo ni pamoja na uvuvi wa mazao ya bahari mfano uokotaji wa tondo, wananchi kuchuma mboga ya pwani, na uwindaji wa ndege.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.